JIJI la Arusha na Mkoa wa Manyara, hali ya hewa ilishachafuka, wingu zito limefunika kufuatia kuuawa kwa kupigwa risasi, mfanyakazi wa Kampuni ya Tanzanite One, Onesmo William Mushi (pichani). |
Mtuhumiwa wa mauaji hayo ni bilionea wa madini, mkazi wa Arusha, Joseph Mwakipesile ‘Chusa’ ambaye ni mfanyabiashara anayemiliki migodi, Mererani wilayani Simanjiro, Manyara.
ONESMO ALIVYOUAWA
Habari zimedai kwamba Onesmo akiwa eneo lake la kazi, mgodini chini, alipigwa risasi mbili kifuani ambazo ziliondoa uhai wake.
Tukio hilo lilitokea saa 8 usiku, Julai 20, mwaka huu, chanzo kikitajwa kwamba ni mgogoro wa kugombea madini.
Imedaiwa kuwa Onesmo, akiwa na wafanyakazi wenzake wa Tanzanite One ambao wamefahamika kwa jina mojamoja, Kennedy na Leonard, walikutana na wachimbaji wadogowadogo hivyo kutokea mvutano wa kimaslahi.
Habari zimedai kwamba miongoni mwa wachimbaji hao wadogo, alikuwepo Chusa ambaye ndiye anadaiwa kufanya mashambulizi dhidi ya Onesmo.
FAMILIA YALIA KUMPOTEZA ONESMO
Julai 25, mwaka huu, Onesmo alizikwa kijijini kwao, Uswaa, Machame, Hai, Kilimanjaro hivyo kuhitimisha safari yake hapa duniani.
Vilio na huzuni vilitanda kipindi chote cha mazishi ya Onesmo, huku sikitiko kubwa likielekea kwa mjane wa marehemu ambaye ameachiwa watoto wawili ambao atawalea bila baba.
Mke wa marehemu, watoto wake na ndugu wengine walikuwa wanyonge muda wote wa mazishi, kuonesha namna walivyoguswa na kifo hicho.
MERERANI YATIKISIKA
Wiki moja baada ya Onesmo kuuawa, wafanyakazi wa Tanzanite One wapatao 200, walilitikisa eneo la Mererani na kusimamisha shughuli zote za uchimbaji madini mpaka wapate tamko la serikali.
Kishindo cha wafanyakazi hao kilisababisha shughuli kusimama hata katika migodi ya wachimbaji wadogo, kwani hasira zilikuwa kali mno.
Awali, wafanyakazi wa Tanzanite One waligoma kufanya kazi wakiitaka menejimenti ya kampuni hiyo kufuatilia haki zote, ikiwemo mtuhumiwa wa mauaji kukamatwa na kufikishwa kortini.
Baadaye, wafanyakazi hao walikusanyika na mabango kisha kushinikiza sheria kuchukua mkondo wake, vilevile wakaituhumu serikali kufumbia macho suala hilo.
Aidha, wafanyakazi hao walibeba mabango yenye ujumbe ambao uliwatuhumu moja kwa moja baadhi ya viongozi wa jeshi la polisi pamoja na wale wa madini Kanda ya Kaskazini kwamba hawaaminiki katika kutenda haki.
MIGODI YAFUNGWA
Kutokana na kifo cha Onesmo, Wizara ya Nishati na Madini, imeifunga kwa muda migodi minne inayozunguka eneo la mgodi wa Kampuni ya Tanzanite One ili kusafisha hali ya hewa iliyochafuka.
Wizara imefanya hivyo kufuatia malalamiko ya wafanyakazi wa Tanzanite One kwamba kifo cha Onesmo kimesababishwa na serikali kulea mgogoro wa mipaka kwa muda mrefu.
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Benjamini Mchwampaka, alisema kuwa migodi iliyofungwa ni ile inayomilikiwa na wafanyabiashara Joseph Mwakipesile ‘Chusa’, Jackson Simon, Abdulhakim Mula pamoja na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Maning’oo.
SERIKALI YACHUKUA HATUA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP Akili Mpwapwa, aliliambia gazeti hili kuwa Chusa alikamatwa yapata wiki mbili zilizopita, baada ya jeshi lake kujiridhisha na tuhuma dhidi yake.
“Tuliona tuhuma dhidi yake zina nguvu ndiyo maana tukamkamata,” alisema Mpwapwa na kuongeza: “Siku tatu zilizopita (kutoka Jumapili iliyopita), alifikishwa mahakamani, akasomewa mashtaka kwa mara ya kwanza na sasa hivi yupo gerezani.
“Sijajua atarudishwa lini mahakamani lakini hii ninayokupa ni taarifa ya uhakika kwamba huyo bwana yupo gerezani. Tulimkamata na kumfikisha mahakamani kama mtuhumiwa wa mauaji, siyo kwa ajili ya kuisaidia polisi.”
TATIZO LA MGOGORO
Kwa mujibu wa taarifa za Mererani, mgogoro wa mipaka kati ya wachimbaji wadogo na Kampuni ya Tanzanite One ni wa muda mrefu.
Imeelezwa kwamba mara kwa mara, wafanyakazi wa kampuni hiyo wamekuwa wakikutana na wachimbaji wadogo mgodini chini, hivyo kuibua mvutano.
Kitendo cha wachimbaji wadogo kukutana mgodini chini na wafanyakazi wa Tanzanite One, kinajulikana kama Mtobozano.
Kwa upande mwingine, imekuwa ikidaiwa kuwa Mtobozano ni lugha ya kulainisha mambo, kwani ukweli ni kwamba ni kitendo cha wachimbaji wadogo kuvamia mgodi wa Tanzanite One na kupora madini.
Imeelezwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaomiliki migodi Mererani, hujipatia fedha haramu, kwa kuiba madini ya tanzanite katika migodi ya Tanzanite One.
Kufuatia hali hiyo, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Uswaa Machame, Robinson Manga, alisema wakati wa ibada ya mazishi ya Onesmo kwamba lazima serikali itafute ufumbuzi wa kudumu kuhusiana na mipaka Mererani.
Mchungaji Manga alisema: “Tatizo la migogoro kati ya wachimbaji wadogo wa madini ya tanzanite na wawekezaji wakubwa limekuwa la miaka mingi, serikali inatakiwa kuangalia upya mipaka na kupata ufumbuzi wa kudumu.”
0 komentar:
Post a Comment